**********************************
Habari hizo zilienea kama moshi jangwani, katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.
'Muhadhiri mkware awahepa makachero baada ya kufumaniwa na mwanafunzi' vilisoma vichwa vya habari.
Baada ya kisa hiki,mamia ya wanafunzi walijitokeza kupasua mbarika kuhusu masaibu yao kutokana na 'alama za ngono'.
Ilitambulika kuwa ni saratani iliyokuwa imetawala katika vyuo vingi,hasa Afrika.
Chini ya heshitegi #SexGrades; waathiriwa wengi walijitokeza na kueleza waliokumbana nayo katika vyuo vyao.
Visa vingi vya kutamausha vilijitokeza na wahadhiri wahusika kutajwa bayana.

Mmoja wapo wa waathiriwa alikuwa ni Charita, ambaye kwa sasa alikuwa Mwanauchumi mtajika.
Alielezea kwa uchungu mkubwa jinsi Abedi, Mchungaji mla kondoo,alivyomfanyia unyama, alipoenda kutafta ushauri kwake.
Charita alikuwa yatima aliyewapoteza wazazi wake kakita mapigano ya kikabila baada ya uchaguzi.
Familia yake ilikuwa moja ya  madodoa yaliyolengwa kuondolewa kulingana na wachochezi wanasiasa.

Babake alikuwa mfanyabiashara aliyenunua shamba katika eneo tofauti na alikozaliwa na kujenga jumba la kifahari.
Walikuwa wanajiweza kimaisha na kuishi maisha ya hali ya juu.
Wakati wa siasa majirani waligeuka na kuwa mahasidi waliowangamiza.
Kisa cha asubuhi hio ya mwaka wa elfu mbili na nane kilimsumbua na kumukoseza usingizi Charita.
Yaliotukia yalijirudiarudia akilini mwake kila alipolala au kutulia.
Alishuhudia kila kitu asijue la kufanya.
Asubuhi hiyo,genge la wenyeji,wakiwemo majirani,walivamia maakazi yao na kuteketeza kila kitu,walikiwemo wamiliki.
Wazazi na ndugu zake waliteketezea kiasi cha kubakia jivu.
Charita aliponea kwa kuwa wakati huo alikuwa amekwenda shambani kutafta matunda.
Duru walizozipiga  zilimkwama kama doda sugu akilini.
Aliokolewa na msamaria mwema aliyemfikisha kwenye makao makuu ya Askofu wa Kikatoliki, walipopewa hifadhi waathiriwa wengi wa mchafuko huo.
Charita alikuwa amemwendea Abedi akimtaka kumwombea na kumshauri kuhusu tatizo la kiakili, lililomwadama asiweze kumakinika masomoni.
Badala yake, Abedi alichukua fursa hiyo na kumnajisi huku akimwonya kuwa,angetoboa unyama huo,basi Abedi angekatiza msaada wake wa masomo uliokuwa ukitolewa kupitia afisi yake.
Charita akawa hana budi ila kutia zii,hadi wakati huu ambapo aliupata mwanya wa kumkabili ibilisi, Mchungaji mla kondoo.
Kidagaa cha Abedi kilikuwa kimemwozea,kwani alipigwa kalamu na kufunguliwa mashtaka.
Kwake Charita,siku njema ilikuwa umefika.
*********************************
Mathangi alifaulu kukwepa mtego wa makachero na kuchania mbuga nchi jirani akitumia 'bodaboda'.

Kwanza, alitorokea mji wa mpakani ambapo alijificha kwa muda kabla ya kuvuka boda kwenda mafichoni.
Nyuma aliwaacha mke na watoto wawili, ambao maisha  yaligeuka kutoka na ukiritimba wa jamii.
Kila walipopita,waliowafahamu waliwasengenya na kuwaangalia kwa kinyaa.
Marafiki waliwakwepa,wakabaki wametengwa kama wagonjwa wa kifafa
Maisha yakawa magumu kwa wanawe katika shule walikosomea.
Wakachekwa na wenzao na kubandikwa majina ya kejeli.
Ilimbidi mama yao kuwatoa shuleni kwa muda,ili kuwataftia shule nyingine.
Maskini wakaubeba msalaba wa dhambi za baba yao.

Kule Uganda, Mathangi alijihusisha na biashara ya kuuza nyama  kijijini alikopewa hifadhi na rafiki yake wa zamani.
Alibadilisha hulka yake kutoka udaktari,ila alilivaa lilelile kabuti jeupe kuuzia nyama.
Alibadilisha jina lake na wenyeji wakawa wanamwita 'daktari',bila kufahamu alikuwa daktari wa ukweli.
Biashara yake ilinawiri mno.
Alinuia kufanya biashara na kukusanya pesa ambazo angezitumia kutorokea ughaibuni,kurejelea kazi yake ya uhadhiri.

***********************************
Suzzanna alisalia hospitalini kwa muda wa miezi miwili.
Kuanguka alikoanguka kulimwacha na jeraha kichwani.
Jeraha ambalo lilimlaza katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa mwezi mmoja.
Alikuwa hajijui wala kujitambua.
Alifanyiwa upasuaji, ambao kwa wakati huu,ulikuwa wa kuondoa damu iliyoganda ubongoni.
Upasuaji ulifaulu na alitarajiwa kupona kabisa.
Wendani wake,Bundi na Chris walisimama naye kidete, wakimtembelea kila wakati.
Ikawa ni zamu ya Bundi kumjali na kumushughulikia rafiki yake.

Rosata alitukia kuwa kiegemezi  cha kutegemewa wakati huo.
Rosata alikuwa na kipawa cha utunzi na uimbaji.
Kila mara akitunga na kumwimbia Suzzanna nyimbo na mashairi ya kumtia moyo na kumuliwaza,akiwa katika sitofahamu kule 'ICU'

"Suzzanna kipenzi,kiumbe uliyeumbika
Kakuumba jalali na urembo kukutunuku.
Kipawa kakubidhi,nayo mengi maarifa.
Ni majukumu maridhawa,alokundea kuyakamilisha.
Nakuembea siha halili,urudi kuendelea
Dunia yakungojea,wema wako kupambia."

Jason alijitolea kugharamia matibabu yote na pia kuhaidi matibabu zaidi kule Marekani.
Kwa Sasa Jason alikuwa mmoja wa wachezaji wakwasi zaidi wa kiafrika kule Marekani.
Alikuwa ameanzisha 'Jason Foundation',kwa madhumuni ya kukuza na kutambua talanta katika watoto Afrika, pamoja na kuwasaidia kupata nafasi za kung'aa Uropa na Marekani.

Hafsa angetoa huduma zake za uwakili kuhakikisha haki ingepatikana kwake Suzzanna na waathiriwa wengine.
Je mkono mrefu wa Sheria ungefaulu  kumchimbua Mathangi alokojificha?

Masaibu yaliyowakabili mkewe Mathangi na malaika wao wawili,yalitoa nafasi kwa Bundi na wenzake, kuwasaidia kupitia kwenye lindi la fedhea walioletewa.

Ama kweli akufaaye kwa dhiki ndio rafiki.

SUZANNAWhere stories live. Discover now