"Enhee! Hivi unaweza kuja wakati wowote unaotaka lakini mimi nikitembea kwa shoga zangu ni hatia..." Rehema alifoka. "Taasubi hii! Mimi nimechoka kuchezwa kama boli. Mara napigwa huku, mara kule, ngoja hapa, mpaka lini?"
Alivyozidi kuongea ndivyo ari yangu ilivyonipanda hata nikahisi damu yangu ikichemka. Koo yangu ilijikaza nikadhani labda kuna jiwe humo lililonipa uchungu kila nilipomeza funda la mate. Macho yangu yalipata joto kama kaa. Nilihisi kana kwamba yalikuwa yakitishia kutoka yalipokuwa yampe mwanamke huyu kichapo alichohitaji.
Naye hakusita kulalamika akisonya na kudonadona hewani kwa kidole hicho kila alipotamka neno la kuashiria. Kila alipohitimisha sentensi alifungua mpya kwa kupigisha makofi yake kama wafanyavyo warembo wa pwani.
Kwa miaka miwili tuliyokuwa tumeoana, sikuwahi kumwona vile. Alikuwa mnyenyekevu, mpole na zaidi niliona mapenzi ya dhati kwake. Alikuwa daima ananitia moyo na kunipa wosia. Alikuwa mwandani tena kipenzi cha moyo wangu.
Siku ile alinifika kooni. Cheche alizozitema ziliniumiza mtima. Kila alichokisema kilinichoma hadi kwenye uboho. Nilitamani kumzaba moja shavuni lakini nguvu za kutekeleza wazo hilo sikuzipata. Ingawa uso wake ulikuwa umesawijika kwa hasira, urembo wake bado ulikuwa dhahiri.
Nywele zake laini zilitulia vyema kwenye kifua chake kama skafu iliyopita mabegani mwake pande zote mbili. Vipuli vyake vilichezacheza kutokana na jinsi alitikisa kichwa chake aliponena. Macho yake yenye kope si haba yalipendeza kila alipopepesa. Mboni za macho yake zilikuwa zinachezacheza na hili lilinihakikishia kuwa bado alinipenda.
"Toka humu mwangu. Iwapo nimekuchosha, haya ondoka basi."
Nafsi yangu ilinisuta nilipoyasikia maneno yaliyokuwa yakitoka kinywani mwangu. Sikutaka anitoke lakini hasira yangu ilinilevya ikanipumbaza. Midomo yangu ilitetemeka nilipojaribu kutaja samahani.
Eti samahani? Samahani ni msamiati wa kike. Ni mwiko kwa mwanaume kulitaja. Atakoseaje mwanaume? Tangu lini akamjibu mkewe? Atakuwaje kiongozi wa mkewe ikiwa hana uhuru wa kufanya atakavyo? Kama nimechelewa kazini akimtafutia mkewe na mwanawe angalau wali mkavu. Ikiwa sijampa uhuru wa kuwatembelea shoga zake alivyowaita, kwani nani angependa mkewe ashiriki udaku wa ploti?
"Phil baby, Phil! Mpenzi nielewe nili..." Rehema alijaribu kunirai. Machozi yalikuwa yanamlengalenga.
"Aha!"
"Phil, leo umenifukuza mie! Naenda kupakia vitu vyangu basi." Rehema aligeuka na kupanda vidato upesi.
"Nyumba yangu hii uione paa!" Nilibweka kwa hamaki na kuutupa mkoba wangu kwenye kochi.
Akililia wembe mpe. Sikuwa mchoyo siku ile. Nilimpa papo hapo. Moyoni nilijihisi mwepesi. Sasa hata hao kina Musa wangetambua mimi siye mnyonge waliyenidhania. Wangeliona ubabe wangu.
Aliporudi kutoka chumbani na begi dogo, ilikuwa dhahiri kwamba alikuwa akilia humo. Kope zake zilikuwa zimeshikana kwa mabunda yenye unyevu. Macho yake yalinitazama kwa huruma na upendo.
"Naondoka. Tafuta mfungwa mwingine. Miye sitaweza." Rehema alijaribu kuigiza hasira.
Sikutaja chochote hata alipou-slam mlango nyuma yake.
"Mwone! Wewe unakwenda hadi manane nami mfungwa wako. Hadi lini?" Niliiga kwa utani.
YOU ARE READING
SAMAHANI
Short Storyswahili love story. A short story. Husband kicks wife out of his house. Will he find another or will he seek after his love?
